Search

Waandishi: Ayiera Elijah Arasa, Dkt. Ontieri James Omari, Dkt. Ayodi Nancy

Ikisiri: Lugha ni kiungo muhimu cha riwaya kwani ni kupitia kwa lugha ambapo mwandishi huyafikia malengo yake ya kisanaa na kuwasilisha ujumbe wake. Suala hili limechangamkiwa na watafiti wengi wa fasihi kote ulimwenguni. Makala hii inajikita katika kuchunguza mchango wa mazingira ya mwandishi katika matumizi ya mafumbo kwenye riwaya mbili za Katama Mkangi: Mafuta na Walenisi. Kwanza, makala hii imebainisha kuwa, wakati ambapo Mkangi alikuwa akiandika riwaya hizi, uhuru wa kuikosoa serikali iliyokuwa mamlakani haukuwepo na kwa hivyo, alilazimika kutumia ufumbaji kuwasilisha ujumbe wake ili kuhepa rungu ya serikali. Pili, alikosomea na waandishi wengine, walimwathiri katika matumizi ya mbinu ya ufumbaji katika Uandishi wake. Tatu, hali ya kisiasa dhidi ya waandishi wakati wa uandishi wake ilimlazimisha kutumia lugha ya ufumbaji ili ichukuane na wakati huo. Aidha, kutokana na makala hii ni dhahiri kuwa Mkangi alitumia mbinu ya ufumbaji kumzindua msomaji kuhusu athari za utabaka, ubepari, unafiki wa viongozi miongoni mwa mengine. Yaliyoshulikiwa kaika makala haya yalilikusanywa kupitia kwa upekuzi wa maandishi na riwaya mbili za Mkangi: Mafuta na Walenisi kwa kuzingatia lugha ya mafumbo. Makala haya ni muhimu kwa kuwa yatawasaidia wasomaji kuelewa kazi hizi za Mkangi zilizoandikwa kimafumbo.  

 Waandishi: Aruba Beatrice Kemunto, Prof. Mohochi Sangai Ernest, Dkt. Ontieri James Omari

 Ikisiri: Lugha ni kipengele muhimu ambacho huwezesha kuwepo kwa mawasiliano miongoni mwa watu. Katika juhudi za kurahisisha uwasilishaji na upokeaji wa ujumbe, ni muhimu kuhakikisha kuwa lugha sahihi imetumiwa. Katika karne hii ya 21 ya mawasiliano ya sayansi na teknolojia, suala la mawasiliano limeshika kasi kubwa kwa kila mtu. Kwa namna hii mawasiliano yamekuwa ni jambo muhimu sana ambalo humwezesha mtu kupashana habari, taifa kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kuhusu matukio, na hata malengo na mikakati iliyojiwekea. Iwapo makosa yatatokea katika maandishi au mazungumzo, mawasiliano kama shughuli kuu ya kibinadamu hayatafaulu. Madhumuni ya makala haya ni kuchanganua makosa ya kisemantiki yanayojitokeza katika mawasiliano andishi ya Kiswahili ya wanafunzi wa shule za upili. Makala haya yametumia nadharia ya Uchanganuzi Makosa (Corder, 1967) kuonyesha kuwa wanafunzi wanaojifunza lugha ya pili hufanya makosa ambayo yanaweza kubainishwa, kuchanganuliwa, kuainishwa na kutathminiwa ili kubainisha mfumo unaofanya kazi. Data ya makala haya ilikusanywa kutoka kwa wanafunzi wa shule za upili hususani kidato cha tatu, kaunti ya Kakamega, nchini Kenya. Mbinu iliyotumiwa katika ukusanyaji wa data ni ya nyanjani (hojaji na mjarabu). Katika kubainisha makosa husika, makala haya yametumia vielelezo mbalimbali kutoka kwa watafitiwa lengwa. Makala haya pia yanatoa mapendekezo ya utatuzi wa makosa yanayojitokeza katika matini za wanafunzi wa shule za upili. Makala haya yatawafaidi walimu wa Kiswahili, wanafunzi wa shule za upili na vyuo vya elimu ya juu katika kurekebisha makosa ya kisemantiki katika matini anuwai.  

 Waandishi: Fridah Oiko Gesare, Dkt James Ontieri Omari, Dkt. Emmanuel Kisurulia Simiyu

 Ikisiri: Mwandishi wa kazi ya fasihi kama mzawa wa jamii anayoindikia, huwa na mbinu mbalimbali za kisanaa anazoweza kutumia katika kuwasilisha mawazo yake kama anavyoyashuhudia katika jamii. Mbinu hizi ni nyingi na hivyo mwandishi hulazimika kufanya uchaguzi wa ile itakayofaa ujumbe anaowasilisha. Uchaguzi huu huathiriwa na jinsi anavyotaka mawazo yake kueleweka na kuleta taathira anayokusudia. Aidha mbinu anayoteua mwandishi sharti iwe ni ile isiyotinga mahusiano ya wanajamii (watawala na watawaliwa). Mojawapo ya mbinu hizo ni kinaya. Kinaya ni mbinu ya kisanaa ambayo hulenga kukuza mawazo kwa njia iliyo kinyume na matarajio. Makala haya yametathmini matumizi ya kinaya katika kukejeli viongozi wa nchi changa za Bara la Afrika ambao katika utendaji kazi duni ambao umezalisha maendeleo yasiyokuwepo. Makala haya yameongozwa nadharia ya Uhakiki wa Kimtindo. Makala haya yamebainisha kwamba Arege ameegemea sana mtindo wa kinaya katika kuwasilisha mawazo yake. Imebainika pia kuwa lengo kuu la kinaya ni kusuta kwa lengo la kuadilisha wanajamii katika kuimarisha viwango vya maendeleo yanayohitajika katika katika sekta mbalimbali. Aidha, kupitia kwa makala haya imebainika kuwa Arege ameegemea sana kinaya ili kukejeli jamii nzima bila kuhujumu mahusiano ya kitabaka yaliyomo katika jamii anayoiandikia. Makala haya yamezingatia kinaya kwa kuegemea nadharia ya Uhakiki wa Kimtindo. 

 Waandishi: Syekei Martha Nyangweso, Dkt. Ayodi Nancy, Prof. Mohochi Ernest Sangai

 Ikisiri: Wasomi na wahakiki wametathmini tanzu mbalimbali kama vile ushairi, riwaya na nyimbo kuhusu kiongozi wa kike.  Lakini utanzu wa tamthilia haujashughulikiwa kwa kina kumpa mhusika huyu sifa anazozistahili.  Wahakiki wengi hawana habari kuwa mhusika huyu ana wadhifa mkubwa katika uongozi wa jamii husika, sio barani Afrika tu, bali duniani kote.  Makala haya yanatathmini uteuzi na athari ya kiongozi wa kike katika jamii husika.  Mbali na makala haya kuangazia uteuzi wa mhusika huyu wa kike yanazamia kuelezea athari aliyo nayo katika jamii kwa ujumla mbali na changamoto anazopitia.  Ni vipi matokeo ya utafiti huu itaongezea idhibati ya mambo muhimu katika fasihi ya lugha ya Kiswahili?

Go to top
Privacy Policy|| Copyright & Permissions